Dkt. Abbasi: Tanzania Ipo Tayari Kuanzisha Utalii wa Anga
Karatu, Arusha
Septemba 19, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya @MNRT_Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi, amefungua mafunzo ya kimkakati kuhusu zao jipya la utalii wa kuangalia vitu vya angani (astrotourism) ili kuwajengea uwezo Watanzania kuvumbua, kuendeleza, kuutangaza na kunufaika na utalii huu unaokua kwa kasi duniani.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya @visitngorongoro, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, @Open_univ_tz Taasisi ya Mafunzo ya Utalii wa Anga (Astrotourism Aotearoa) ya nchini Autoroa (New Zealand), na mashirika ya Smithsonian Astrophysical
Observatory (SAO) kutoka Chuo Kikuu cha Harvard na Dark Sky International ya Marekani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Abbasi amesema “si tu Tanzania iko tayari kwa utalii huo mpya na ikiwa moja ya nchi duniani zenye maeneo mengi yenye anga safi lenye rangi ya samawati, na nyota na vitu vingine vya angani vyenye mng’ao munawari tunataka kuwa kinara wa utalii huu mpya,” alisema Dkt. Abbasi.
Taasisi za @bookingcom ya nchini Uholanzi inayotoa huduma za makazi na malazi kwa mamilioni ya watalii kwa mwaka (ikiwa imehudumia watalii bilioni 6.8 tangu mwaka 2010), na ile ya TheTravel ya nchini Kanada mtawalia, zinaeleza katika utafiti wa hivi karibuni kuwa asilimia 62 ya wateja wao walieleza kutaka kufanya utalii wa anga kila wanaposafiri kutalii na kwamba kufikia mwaka 2030 utalii huu utazalisha mapato ya Dola za Marekani Bilioni 5.8.